Matthew 5

1Yesu alipo uona umati, akaondoka na kuelekea Mlimani. Alipokuwa ameketi chini, wanafunzi wake wakaja kwake. 2Akafunua kinywa chake na akawafundisha, akisema, 3“Heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao. 4Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa.

5Heri wenye upole, maana watairithi nchi. 6Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa. 7Heri wenye rehema maana hao watapata Rehema. 8Heri wenye moyo safi maana watamwona Mungu.

9Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu. 10Heri wale wanaoteswa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao.

11Heri ninyi ambao watu watawatukana na kuwatesa, au kusema kila aina ya ubaya dhidi yenu kwa uongo kwa ajili yangu. 12Furahini na kushangilia, maana thawabu yenu ni kubwa juu mbinguni. Kwa kuwa hivi ndivyo watu walivyo watesa manabii walioishi kabla yenu.

13Ninyi ni chumvi ya dunia. Lakini kama chumvi imepoteza ladha yake, itawezaje kufanyika chumvi halisi tena? Kamwe haiwezi kuwa nzuri kwa kitu kingine chochote tena, isipokuwa ni kutupwa nje na kukanyagwa na miguu ya watu. 14Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojegwa juu ya mlima haufichiki.

15Wala watu hawawashi taa na kuweka chini ya kikapu, bali kwenye kinara, nayo yawaangaza wote walio ndani ya nyumba. 16Acha nuru yenu iangaze mbele za watu kwa namna ambayo kwamba, wayaone matendo yenu mema na kumtukuza Baba yenu aliye mbinguni.

17Msifikiri nimekuja kuiharibu sheria wala manabii. Sijaja kuharibu lakini kutimiza. 18Kwa kweli nawaambia kwamba mpaka mbingu na dunia zote zipite hapana yodi moja wala nukta moja ya sheria itaondoshwa katika sheria hadi hapo kila kitu kitakapokuwa kimekwisha timizwa.

19Hivyo yeyote avunjaye amri ndogo mojawapo ya amri hizi na kuwafundisha wengine kufanya hivyo ataitwa mdogo katika ufalme wa mbinguni. Lakini yeyote azishikaye na kuzifundisha ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. 20Kwa maana nawaambia haki yenu isipozidi haki ya waandishi na Mafarisayo, kwa vyovyote vile hamtaingia katika ufalme wa mbinguni.

21Mmesikia ilinenwa zamani kuwa, “usiue” na ‘yeyote auaye yuko katika hatari ya hukumu.’ 22Lakini nawaambia yeyote amchukiaye ndugu yake atakuwa katika hatari ya hukumu. Na yeyote amwambiaye ndugu yake kuwa, ‘Wewe ni mtu usiyefaa!’ atakuwa katika hatari ya baraza. Na yeyote asemaye, ‘Wewe mjinga!’ atakuwa katika hatari ya moto wa jehanamu.

23Hivyo kama unatoa sadaka yako katika madhabahu na unakumbuka kuwa ndugu yako ana jambo lolote dhidi yako, 24iache sadaka mbele ya madhabahu, kisha shika njia yako. Kapatane kwanza na ndugu yako, na kisha uje kuitoa sadaka yako.

25Patana na mshitaki wako upesi, ukiwa pamoja naye njiani kuelekea mahakamani, vinginevyo mshtaki wako anaweza kukuacha mikononi mwa hakimu, na hakimu akuache mikononi mwa askari, nawe utatupwa gerezani. 26Amini nawaambieni, kamwe hutawekwa huru hadi umelipa senti ya mwisho ya pesa unayodaiwa.

27Mmesikia imenenwa kuwa, ‘Usizini.’ 28Lakini nawaambieni yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye moyoni mwake.

29Na kama jicho lako la kulia linakusababisha kujikwaa, ling’oe na ulitupe mbali nawe. Kwa kuwa ni afadhali kiungo kimoja katika mwili wako kiharibike kuliko mwili mzima kutupwa jehanamu. 30Na kama mkono wako wa kuume unakusababisha kujikwaa, ukate kisha uutupilie mbali nawe. Maana ni afadhali kiungo kimoja katika mwili wako kiharibike kuliko mwili mzima kutupwa jehanamu.

31Imenenwa pia, yeyote amfukuzaye mkewe, na ampe hati ya talaka.’ 32Lakini mimi nawaambia, yeyote anaye mwacha mke wake, isipokuwa kwa kwa sababu ya zinaa, amfanya kuwa mzinzi. Na yeyote amuoaye baada ya kupewa talaka afanya uzinzi.

33Tena, mmesikia ilinenwa kwa wale wa zamani, ‘Msiape kwa uongo, bali pelekeni viapo vyenu kwa Bwana.’ 34Lakini nawaambia, msiape hata kidogo, ama kwa mbingu, kwa sababu ni enzi ya Mungu; 35wala kwa dunia, maana ni mahali pa kuweka kiti cha kukanyagia nyayo zake, ama kwa Jerusalemu, maana ni mji wa mfalme mkuu.

36Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37Bali maneno yenu yawe, ‘Ndiyo, ndiyo, Hapana, hapana.’ Kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.

38Mmesikia imenenwa kuwa, ‘Jicho kwa jicho, na jino kwa jino.’ 39Lakini mimi namwambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akikupiga shavu la kulia mgeuzie na jingine pia.

40Na kama yeyote anatamani kwenda na wewe mahakamani na akakunyang’anya kanzu yako, mwachie na joho lako pia. 41Na yeyote akulazimishaye kwenda naye maili moja, nenda naye maili mbili. 42Kwa yeyote akuombaye mpatie, na usimwepuke yeyote anayehitaji kukukopa.

43Mmesikia imenenwa, ‘Umpende jirani yako, na umchukie adui yako.’ 44Lakini nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanao waudhi, 45Ili kwamba muwe watoto wa baba yenu aliye mbinguni. Kwa kuwa anafanya jua liwaangazie wabaya na wema, na anawanyeshea mvua waovu na wema.

46Kama mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Kwani watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47Na kama mkiwasalimia ndugu zenu tu mwapata nini zaidi ya wengine? Je!, Watu wa mataifa hawafanyi vivyo hivyo? Kwa hiyo yawapasa kuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

48

Copyright information for SwaULB